KUMEKUCHA TOC , MWAKALEBELA APANIA MAKUBWA
Bw Mwakalebela
Mwakalebela amwaga sera za kuvutia
*Asema kama niliweza TFF siwezi kushindwa TOC
*Aahidi ushirikiano wa karibu na Serikali, wadau wa michezo
*Ashangaa kukosekana kwa medali za Olimpiki tangu 1980
*Aahidi uwazi kwenye mapato na matumizi ya TOC
SIKU chache baada ya kupitishwa kugombea nafasi ya Katibu
Mkuu wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC), Katibu Mkuu wa zamani wa
Shirikisho la Soka nchini (TFF) Frederick Mwakalebela jana alizindua kampeni
zake kwa kishindo na kuahidi kurejesha heshima ya nchi kwenye michezo
kimataifa.
Akizungumza na waandishi wahabari jijini Dar es Salaam jana,
Mwakalebela alisema ni aibu kwa nchi yenye idadi ya watu zaidi ya milioni 40 na vipaji
kibao kama Tanzania kukosa medali kwenye michezo mikubwa kama ya Olimpiki kwa
zaidi ya miaka 30 sasa.
“Olimpiki ni mashindano makubwa yanayojumuisha michezo
mbalimbali, lakini tangu mwaka 1980, pamoja na kupeleka wanamichezo kwenye
mashindano hayo, hatujawahi kupata medali hata moja,” alisema.
Akiwa makini kutopeleka
lawama kwa uongozi wa TOC uliopita, Mwakalenela alisema kilichosababisha
kupatikana kwa medali mwaka 1980 huko Moscow, Urusi (USSR) ni mfumo mzuri wa
maandalizi ya timu ambapo timu hiyo ilifanya maandalizi ya mwaka mzima kwa
kufanya ziara mikoani na nje ya nchi.
“Kwanini siku hizi inashindikana kufanya hivyo? Ni ukosefu
wa ubunifu, na ndio maana ninagombea ili kuleta mawazo mapya michezoni.
Nikiingia ofisini kazi yangu ya kwanza itakuwa ni kuiweka TOC karibu na wadau
wakubwa wa michezo ambao ni Serikali, vyombo vya habari, makampuni ya biashara,
majeshi, shule, vyuo na taasisi mbalimbli binafsi.
“Ndani ya miezi mitatu tu wadau hao watakuwa ‘marafiki’ wa
TOC na maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 2016 huko Rio de Janeiro,
Brazil yataanza mara moja. Tukikosa medali mwaka huo, basi ni lazima tutapata
mwaka 2020,” alisema kwa kujiamini.
Akijibu maswali mbalimbali ya waandishi, Mwakalebela
aliyefanya kazi kwa ufanisi mkubwa akiwa TFF, alisema TOC mpya itakaa na Rais
Jakaya Kikwete na kumwomba kabla hajamaliza muda wake wa uongozi serikalini
awaachie wanamichezo wa Tanzania kumbukumbu ya Kijiji cha Olimpiki.
Alisema kuwapo kwa kijiji hicho kutawapa nafasi vijana wenye
vipaji nchini kuonyesha uwezo wao na kutokana na wao, ndipo timu bora ya taifa
itakayokuwa ikiiwakilisha nchi kwenye michezo mbalimbali itakuwa ikipatikana.
“Tutashirikiana na wizara husika, balozi za kimataifa,
Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) yanayotoa nafasi za mafunzo (scholarship
awards) na organaizesheni za michezo za kimataifa kuwatafutia wanamichezo wetu
nafasi za masomo na mafunzo nje ya nchi.
“Hili liwahi kufanyika na watu kama kina Filbert Bayi,
Suleiman Nyambui na Mwinga Mwanjala walifaidika sana na mpango huu na kisha
kuliletea taifa letu sifa kubwa michezoni,” alisema Mwakalebela ambaye kwenye
kinyang’anyiro hicho atapambana na Bayi anayetetea nafasi ya Katibu Mkuu wa
TOC.
Kikubwa zaidi, Mwakalebela alisema mapato na matumizi ya TOC
yatawekwa wazi ili kile kidogo kinachopatikana, kikijumlishwa na kingine kutoka
serikalini na kwa wadau, kifanye kazi iliyokusudiwa ya kuendeleza michezo
nchini.
TOC ndio msimamizi na mlezi wa vyama na mashirikisho ya
michezo nchini na ndio waandalizi wa timu za taifa zinazoshiriki michezo ya
Olimpiki, Jumuiya ya Madola na Michezo ya Afrika (All African Games).
No comments:
Post a Comment